Mwanzo Kuandaa Shamba Mbegu & Kupanda Kutunza Shamba Kuvuna & Kuhifadhi Maswali | Majadiliano Mawasiliano & Ushauri Uza na Kununua

Kuvuna na Kuhifadhi

Sehemu hii tutazungumzia; Kuvuna Mahindi Yaliyokauka, Maandalizi ya Kuvuna, Njia za Kuvuna, Kuhifadhi Mahindi, Teknolojia za kuhifadhi Mahindi, Faida za njia za Kisasa kuhifadhi Mahindi, Sifa za Chumba cha kuhifadhi Mahindi, Usafi wa Jumla katika Kuhifadhi, Wadudu katika kuhifadhi, Sumu ya Mycotoxins, na Njia Zingine za Kudhibiti Fangasi.

Sumu ya Mycotoxins

Sumu hii huweza kusababisha kansa na ukuaji dhaifu kwa watoto na huweza kusababisha vifo pia. Binadamu na wanyama wengine huathirika wanapotumia mazao yenye sumu ya Mycotoxins. Sumu hii haiwezi kuondoka kwenye chakula kwa njia za kawaida za upikaji chakula.

Visababishi vya Mcotoxins
Kuna vitu kadhaa vinavyosababisha sumu ya Mycotoxins kuzalishwa. Baadhi ya hivyo ni; mmea kuwa dhaifu au kuwa katika hali ya kuweza kuathiriwa na fangasi, hali ya joto, kiwango cha unyevunyevu na kuharibika kwa mbegu kutokana na kuingiliwa na wadudu.

Kuzuia Sumu ya Mycotoxins
Fangasi wazalishao sumu huweza kushambulia mazao yako kabla hayajavunwa, wakati unapovuna, baada ya kuvuna na wakati umeyahifadhi. Kiujumla, kuzuia fangasi na sumu yake ya mycotoxins kunahusisha hatua tatu zifuatazo;

Hatua ya Kwanza
Hii ni hatua ambapo juhudi hufanyika kabla mazao hayajaathiriwa na fangasi na sumu ya mycotoxins. Katika hatua hii mazingira hutengenezwa ili fangasi wasipate mazingira mazuri kustawi. Hii ina husisha;
  • Kuzalishwa kwa mbegu za mazao kama mahindi ambazo hazitaweza kuathiriwa na hao fangasi
  • Dhibiti fangasi wabaya kwa kutumia fangasi wa zao la kupandwa
  • Pangilia muda unaofaa wa kabla ya kuvuna, wakati wa kuvuna na baada ya kuvuna
  • Punguza unyevunyevu wa mazao au mbegu baada ya kuvuna na wakati wa kuhifadhi
  • Hifadhi mazao yako kwenye mazingira ya baridi kila inapowezekana
  • Tumia kemikali za kuzuia na kudhibiti kuongezeka kwa fangasi
  • Dhibiti wadudu kwenye mazao yaliyohifadhiwa kwa kutumia kemikali zilizoidhinishwa
Hatua ya Pili
Kama kuna fangasi wametokea katika hatua za awali, hatua hii ifanyike kuwaondoa hao fangasi au kukua kwake kusimamishwa ili kuzuia kusambaa.
  • Zuia kukua kwa fangasi kwa kukausha tena mazao
  • Ondoa mbegu au punje au mazao yaliyoathirika na fangasi
  • Ondoa sumu ya mycotoxins au wafanye fangasi wasiweze kufanya kazi
  • Hifadhi mazao sehemu ambayo fangasi hawawezi kustawi
Hatua ya Tatu
Ikitokea mazao yameathirika sana na fangasi wa sumu, hatua ya kwanza na ya pili haziwezi kufaa. Kinachoweza kufanywa katika hatua hii ni kuzuia au kupunguza hao fangasi na sumu yake nyingi kwenye mazao kuingia kwenye chakula na mazingira yetu. Hapa inashauriwa;
  • Haribu mazao yote vizuri
  • Ondoa sumu kwenye mazao au punguza sumu kwenye mazao ili ibaki kidogo sana
Mhindi ulioathiriwa na sumu ya Mycotoxins Mahindi yaliyoathiriwa na sumu ya Mycotoxins