Mwanzo Kuandaa Shamba Mbegu & Kupanda Kutunza Shamba Kuvuna & Kuhifadhi Maswali | Majadiliano Mawasiliano & Ushauri Uza na Kununua

Kuvuna na Kuhifadhi

Sehemu hii tutazungumzia; Kuvuna Mahindi Yaliyokauka, Maandalizi ya Kuvuna, Njia za Kuvuna, Kuhifadhi Mahindi, Teknolojia za kuhifadhi Mahindi, Faida za njia za Kisasa kuhifadhi Mahindi, Sifa za Chumba cha kuhifadhi Mahindi, Usafi wa Jumla katika Kuhifadhi, Wadudu katika kuhifadhi, Sumu ya Mycotoxins, na Njia Zingine za Kudhibiti Fangasi.

Usafi wa Jumla katika Kuhifadhi

Chumba au nyumba au jengo la kuhifadhi mazao kama mahindi na mazingira yake inapaswa viwe katika hali safi na salama ili mazao yabaki kuwa salama na bora. Ili kufanikisha hili, zingatia yafuatayo;
  • Safisha vizuri sehemu ya kuhifadhi mazao yako kabla na baada ya kuyahifadhi
  • Sakafu, ukuta, na dari/ paa visafishwe mara kwa mara kuondoa vumbi, tandabui na uchafu mwingine
  • Wakati wa kusafisha funika mazao yako na mifuko mikubwa ili yasichafuke
  • Maeneo jirani na ulipohifadhi mazao yako paondolewe nyasi, magugu na vichaka ili kupunguza uwezekano wa kuwa sehemu ya mazalia na kujificha kwa wanyama kama panya na wadudu haribifu
  • Usitupe uchafu kama mabaki ya chakula jirani na ulipohifadhi mazao ili kupunguza uwezekano wa hiyo sehemu kuwa kimbilio la wadudu na wanyama kama panya
  • Weka mitego ya panya kila inapowezekana
  • Fukizia (fumigate) kudhibiti wadudu haribifu. Hakikisha mtaalamu aliyethibitishwa kwa kazi hiyo
  • Hakikisha madirisha na milango ya ghala la mazao vimefungwa muda wote na vifunguliwe kipindi kile tu inapotakiwa
  • Sehemu za kupitishia hewa za ghala lako ziwe na nyavu zinazoweza kuzuia wadudu, ndege na wanyama kama panya
  • Ghala la mazao liwe kwa ajili ya kuhifadhi mazao tu, vitu vingine ambavyo sio mazao vihifadhiwe chumba au sehemu ingine
  • Usihifadhi mahindi sehemu moja na kemikali za shambani au mafuta taa/ dizeli/ petrol au vitu ambavyo ni hatari au sumu kwa binadamu au wanyama wengine
  • Epuka moto eneo la kuhifadhi mazao. Kusiwepo na uvutaji sigara eneo hilo na vitu vinavyoshika moto haraka visihifadhiwe jirani au kwenye ghala la chakula
  • Ikitokea ghala lina mazao tofauti tofauti, kila zao lifungwe au liwekwe kwenye mifuko tofauti tofauti kuepuka kuchanganya mazao na kuzuia maambukizano ya magonjwa au wadudu